04 December 2005

Gertrude Ibengwe Mongella.

Kama kuna wanawake wa kitanzania ambao wameweza kuionyesha dunia kwamba Tanzania nayo ina wanawake wa shoka, basi Mama Gertrude Mongella naye yumo tena katika namba ya juu, hakosi katika namba tatu bora za mwanzo...nani anabisha? Mama huyu ambaye ni mwanasiasa, mwalimu, mwanaharakati, mke na mama wa watoto wanne, ndiye yule aliyeuongoza mkutano wa nne wa dunia kuhusu wanawake uliofanyika Beijing China mwaka 1995. Na ni huyu huyu ambaye ni rais wa kwanza wa bunge la afrika lililoundwa mwaka 2004. Ndugu wasomaji wangu naomba mjue kwamba bunge hili si la kina mama peke yake, ni bunge mchanganyiko. Kwahiyo mwanamama huyu kitendo cha kuwabwaga wanaume wote wa Afrika tena katika uchaguzi wa mara ya kwanza si kitu masihara kabisa.

Kabla sijaendelea zaidi kuwapasha juu ya mambo ambayo mama huyu ameshawahi kuyafanya, ningependa niwadokeze kidogo juu ya maisha yake binafsi.

Mama Gertrude Mongella alizaliwa katika kisiwa cha Ukerewe, mkoani Mwanza mwaka 1945 akiwa ni mmoja kati ya watoto wanne katika familia yao. Baba yake Patrice Magologozi alikuwa ni mjenzi, fundi seremala na mwanaharakati akikabiliana na siasa za mkoloni. Mama yake Bibi Nambona alikuwa ni mkulima stadi. Alizaliwa kipindi ambacho ubaguzi kati ya watoto wa kike na wakiume katika jamii yao ulikuwa umeshika hatamu, wanawake walizuiliwa mambo mengi, mfano kuongea mbele ya wanaume, kula vyakula baadhi ya vyakula au sehemu zilizonona za nyama, mfano mapaja ya kuku,firigisi mayai na vinginevyo vingi. Gertrude aliliona hili na rohoni mwake hakukubaliana nalo kabisa, lakini anamshukuru sana baba yake ambaye alikuwa akimtia moyo na kumwambia asifungwe na hizo mila na desturi ale anachotaka, aseme anapoona pana ukweli na shule atakwenda.

Alipokuwa na umri wa miaka 12, alianza shule iliyokuwa ikiendeshwa na watawa wa Maryknoll Nuns, Shule hii ilikuwa na malengo ya kuwaelimisha na kuwanyanyua watoto wa kike. Na hii ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kusafiri toka azaliwe.

Baadaye alijiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam ambako alipata Shahada ya elimu. Mwaka 1975 aliingia katika siasa na kuwa mwanachama katika Baraza la kutunga sheria la Afrika Mashariki (EALA).

Tangu wakati huo, amekuwa akishikilia nafasi nyingi za uongozi katika Chama tawala na Serikali ya Tanzania, na nje ya nchi bonyeza hapa usome mwenyewe. Na kwa baadhi ya mahojiano ambayo amekwisha yafanya bonyeza hapa na hapa usome, na hapa umsikilize.

Watanzania hatuna budi kushukuru kuwa na mwanamke jasiri na muwezaji wa mambo kama huyu. Gertrude Mongella ni mtu asiye tishika na ndio sababu hata dunia imeweza kumuona. Na baada ya kumfuatilia sana nimegundua jambo moja, si mtu anayekurupushwa na matokeo ya jambo, ni mtu anayeangalia nini kiini au chanzo cha jambo hilo. Mfano ni pale alipozungumzia ya umaskini na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika bara la Afrika. Alisema kwamba" hebu tujiulize waafrika wengi wanaopigana utakuta wanamiliki silaha bora na za gharama mno, lakini mwafrika huyo huyo hana pesa hata ya kuweza kumnunulia mwanae kalamu!! Sasa hapo ujue lipo jambo.. ninani anayempa mwafrika huyu hizo silaha?? ..huyo ndiye wa kusakamwa kwani kama angekuwa na nia nzuri basi angempa kalamu au nyenzo za kufanyia kazi. Hebu usiache kumsikiliza katika kiungo nilichokuwekeeni hapo juu.

Zidumu fikra za Mama Mongella.

4 Comments:

At Tuesday 6 December 2005 at 09:31:00 GMT, Blogger mwandani said...

Kazi nzuri. Baada ya miaka michache nikitaka kujua habari za akina mama wa Afrika ambao kwamba, basi nitakuja kwenye tovuti yako nipate elimu. Ahsante sana.
- Mwandani

 
At Tuesday 6 December 2005 at 23:58:00 GMT, Blogger Jeff Msangi said...

Nakubaliana na Mwandani.Kazi yako ni imara na muhimu.Wanawake kama Mama Mongela na wengineo ni mfano wa kuigwa miongoni mwa wanawake na hata wanaume pia.Kumbuka tunaongelea dunia ya usawa wa kijinsia.Ila,Ila,hili la zidumu fikra zake sikubaliani nalo.Zitadumu kama zitabakia kuwa endelevu kama sasa.Zikibadilika basi nitaomba tusaidiane kuzisitisha!

 
At Thursday 29 December 2005 at 10:08:00 GMT, Blogger Fikrathabiti said...

Dada mija nakuomba sana kama utaweza kunitafutia historia ya Bi hellen kidjo bisimba,mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu(LHRC).

Ningefurahi pia kama ungeweza kuainisha her "LEADERSHP QUALITIES" ambazo unadhani anastahili kusemewa kua anazo.

Au una weza kunitafutia kiongozi yoyote mahiri katika taasisi zisizo za kiserikali kama Rakesh patel wa HAKI ELIMU au wengineo na uniainishie sifa zao!

 
At Friday 30 December 2005 at 09:48:00 GMT, Blogger Mija Shija Sayi said...

Sawa Fikra thabiti, ombi lako limefika.

 

Post a Comment

<< Home